Connect with us

Habari za Kimataifa

BASI LA MAN UNITED NI NDEGE INAYOTEMBEA ARDHINI

WANAPOKUWA nje ya Jiji la Manchester, mara nyingi huwa wanasafiri kwa kutumia treni au ndege kwenda uwanjani, lakini wanapokuwa kwenye ardhi ya nyumbani na miji mingine kadhaa ya England wamekuwa na kawaida ya kutumia basi lao binafsi.

Basi hilo ambalo lilitengenezwa nchini Ubelgiji aina ya TDX27 ASTROMEGA, limekuwa maarufu kwa kuwa linatumiwa na kikosi cha Manchester United hasa katika safari za kuelekea uwanjani.

Siyo mara ya kwanza kwa makala ya basi hilo kuandikwa, lakini kutokana na linavyoboreshwa na lilivyo gumzo ni kawaida kuliona kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

Uzuri wa basi hilo mara kadhaa umesababisha mashabiki wa Man United wataniwe na wenzao kuwa sababu ya timu yao kupenda ‘kupaki basi’ sana uwanjani ni kwa kuwa hata nje ya uwanja wana basi zuri.

 

Msemo wa kupaki basi uwanjani unawakilisha jinsi ambavyo timu hiyo katika kikosi cha sasa ambavyo imekuwa na mbinu nyingi za kucheza kwa kujilinda zaidi kuliko kushambulia, ndiyo maana kunaitwa kupaki basi.

Mastaa wa timu hiyo mfano, Paul Pogba, Marcus Rashford na Romelu Lukaku wamewahi kushea mara kadhaa picha na video wakiwa ndani ya basi hilo la kifahari ambalo oda yake iliagizwa maalum kwa Manchester United.

Uwepo wa basi hilo ni mwendelezo wa klabu hiyo kuthibitisha kuwa wao ni klabu kubwa na hata wachezaji, makocha na watu wao wote wanatakiwa wawe wa daraja la juu.

Basi hilo ambali gharama yake ni pauni 400,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.1) limegawanyika sehemu mbili, juu na chini na kwa jinsi lilivyo na urembo mwingi na madoido ya gharama linafananishwa na ndege.

Lina urefu wa futi 13 kutoka chini kwenda juu, urefu wa nyuma na mbele ni futi 46.27 na lina upana wa futi 8.36, mara nyingi linapokuwa na wachezaji, kasi yake huwa haitakiwi kuzidi spidi 70.

Kumbukumbu za wengi ni tukio lililotokea mwaka 2016 wakati basi hilo liliposhambuliwa na mashabiki wa West Ham United wakati likielekea uwanjani kwa ajili ya mchezo baina ya timu hizo jijini London.

Basi hilo lilishambuliwa kwa chupa na vitu vingine vilivyoelekezwa kwenye vioo, lakini wachezaji na wengine waliokuwemo ndani hawakuumia kwa kuwa vioo vilivyopo ni vigumu na vilivunjika vile vya juu lakini vile vya ndani viliendelea kubaki imara.

Ndani ya basi hilo, kuna jumla ya siti 45, sehemu ya juu ya basi hilo kuna siti 29 na chini kuna siti 16, ambapo kwenye siti zote kuna meza pamoja na runinga kwa kila siti. Katika kila siti mchezaji anaweza kubadili chaneli anayotaka.

Viti vya basi hilo ni vilaini na vinamfanya kila anayekaa kuwa kwenye hali ya utulivu, ‘matirio’ yake yalitengenezwa nchini Italia.

Kuna vifaa vya redio ambapo mkaaji anaweza kubadili chaneli yoyote anayotaka ambayo inapatikana katika maeneo husika. Vifaa hivyo vina uwezo wa kupokea DVD na sauti inaweza kuunganishwa kusikiliza kile kinachotokea kwenye runinga.

Basi hilo lina mtandao maalum wa ‘internet’ ambao unawawezesha walio ndani kuitumia kwa kupitia mfumo wa WiFi. Kila basi linapoanza safari kunakuwa na vitafunwa vyepesi.

Katika sehemu ya chini ya basi hilo kuna sehemu ya jiko ambapo wakiamua kupika wanaweza kufanya hivyo na kama kuna chakula basi kinahifadhiwa maeneo hayo.

Kuna nguo maalum za wapishi ambazo gharama zake ni pauni 770 (Sh milioni 2.2) kwa kila moja, kuna kifaa cha kupashia vitu moto na kupikia (microwave) ambacho gharama yake ni pauni 630 (Sh milioni 1.8) na mashine maalum ya kutengenezea kahawa yenye gharama ya pauni 540 (Sh milioni 1.6).

Mbali na hapo, jikoni kuna jokofu, sehemu ya kunawia, kifaa cha kuchemshia maji ya moto na vifaa vingine vidogo vidogo.

Upande wa pembeni katika kila siti kuna vioo maalum vya kuzuia kitu kigumu kumfikia mtu aliyekaa, mfano chupa ikirushwa.

Vioo vya basi hilo ni vya giza na ni vigumu kwa mtu aliye nje kuona kinachoendelea kwa ndani, ndiyo maana hata wakati waliposhambuliwa na mashabiki wa West Ham walipata nafuu kwa kuwa walikuwa hawaonekani kwa ndani.

Maliwato ya basi hili ni kama yale ya kwenye ndege, kuna choo kidogo na sehemu ya kunawia na mtu anaweza kuoga kabisa.

Pamoja na hivyo, basi hilo limekuwa likitumika katika shughuli nyingine za michezo na siyo kuwapeleka wachezaji uwanjani tu wakati wa mechi.

Mara nyingi ni kawaida kuona makocha na manahodha wa timu hiyo wakikaa sehemu ya chini ya basi hilo wakati wachezaji wengine hasa wanaotakiwa kuanza kikosi cha kwanza wanakaa juu.

Staa mwingine wa United ambaye amekuwa akipiga picha mara kadhaa akiwa ndani ya basi hilo ni Jesse Lingard ambaye amewahi kujirekodi hadi video mara kadhaa na kusambaza kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Kawaida basi hilo limekuwa likiendeshwa na dereva mmoja katika safari nyingi za timu hiyo, kinyume na hapo ni hadi anapokuwa na dharura ndipo anapewa dereva mwingine.

Kingine ni kuwa dereva anapokuwa ameibeba timu, njia za wapi basi litapita zinapangwa na uongozi chini ya katibu mkuu wa klabu na dereva hatakiwi kubadili ‘ruti’ hata moja labda kwa ruhusa maalum.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Habari za Kimataifa