Usajili

BAADA YA LIPULI KUJA JUU, TFF YASEMA INAWEZEKANA SALAMA KUICHEZEA YANGA

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Wilfred Kidao amezungumzia sakata la usajili wa mshambuliaji wa Lipuli, Adam Salamba ambaye anahitajika kwenye kikosi cha Yanga.

Yanga ilitoa taarifa kuwa imetuma maombi ya kumhitaji mchezaji huyo kwa muda kwa ajili ya michuani ya kimataifa ambapo wao wanashiriki katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Baada ya Yanga kuweka maombi yao hadharani, mmoja wa viongozi wa Lipuli alijitokeza na kusema kuwa wao hawapo tayari kumuachia mchezaji huyo kwa muda kwa kuwa bado wanamhitaji.

Kidao amefafanua hivi kuhusu suala hilo kikanuni:

“Ukisoma kanuni za ligi yetu ya Vodacom kuna kipengele kinairuhusu TFF kutoa leseni wakati wowote kwa kuzingatia maslahi ya timu inayowakilisha kwenyemashindano ya kimataifa.”

“Yote hayo lazima yafanyike kwa  mujibu wa makubaliano kati ya timu aliyokuwa anacheza mchezaji dhidi ya timu anayokwenda kuichezea ambayo inashiriki mashindano ya kimataifa lakini kuwe kuna mazingira maalum ya kuweza kufanikisha jambo hilo.

“Kwa hiyo kanuni zetu za ligi kuu zipo wazi kwa jambo hilo, tumepata copy kutoka Yanga kwamba wanamuomba Salamba lakini hawajatuambia kama wameshakubaliana na Salamba ili TFF tujue hatua ambazo tunaweza kuwasaidia Yanga kulingana na kanuni za Caf ili waweze kuwatumia hao wachezaji ambao wanawahitaji.”

“Tutakapokuwa tayari tutawashauri Yanga ni nini ambacho wanaweza kufanya ili waweze kutimiza azma yao pamoja kwamba kanuni zetu za ligi kuna kipengele kinatoa mazingira maalum kuweza kutoa leseni kwa mchezaji ili aweze kuwakilisha klabu ambayo inacheza mashindano ya kimataifa na tuliweka kwa makusudi maalum.”