Usajili

AMMY NINJE ALIPASWA KUJIVUNIA UWEPO WA KABWILI

JANA April 13, timu yetu ya Taifa chini ya miaka 20, Ngorongoro Herous, walishuka dimbani kucheza na vijana wenzao wa Mali katika mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya vijana wenye umri huo Afrika.

Katika mchezo huo, tulioshuhudia mabadiliko ya eneo la mlinda lango akiachwa nje kipa wa timu hiyo Ramadhani Kabwili na kuanza kipa mwingine Abdultwalib Mashery ambaye kiufupi alikuwa na makosa mengi dakika tisini za mchezo.

Ammy Ninje anachokifanya naweza kusema ni kuwatafuta Watanzania lawama kwani hakuna asiyefahamu ubora wa Kabwili na exposure aliyoipata tangu Serengeti Boys hadi sasa katika klabu yake ya Yanga kwa lugha nyingine tunaweza kusema kijana amekwiva.

Natambua kuwa Kocha anauwezo wa kupanga kikosi atakacho ila kwa hili nadhani Ninje alitumia mabavu na kutaka kuonesha kuwa anasauti kubwa kwa timu hiyo, hatukatai ni haki yake ila alipaswa kusoma na alama za nyakati na ajivunie kuwa na mchezaji kama Ramadhani Kabwili mwenye uzoefu wa kutosha.

Tumefungwa mabao 2-1 ambayo ni magoli dhaifu sana kuruhusu tena katika ardhi ya nyumbani yote haya yalionesha kuwa kipa huyo hakuwa na uzoefu wa kutosha kuweza kusoma ubora wa wapinzani na makosa makubwa yalikuwa katika kuanzisha mipira kutoka golini kwake.

Unaikumbuka Serengeti Boys iliyokuwa chini ya Bakari Shime? wengi ni hawa vijana wa Ngorongoro na walikuwa wanacheza soka la kuvutia kuliko sasa chini ya shujaa Ammy Ninje, mwenye jazba nyingi na maamuzi ya mlipuko.

Kwa matokeo haya nadhani ana deni kubwa kwa Watanzania wenye imani na timu zao za vijana ila hatuwezi kumlaumu Ninje tuwalaumu waliompa nafasi na kutuaminisha ni shujaa namba mbili baada ya Mbwana Samatta.