Usajili

BEKI KISIKI AZAM FC AFUNGWA HOGO, SASA KUWA NJE YA UWANJA KWA WIKI SITA

Beki kisiki wa kati wa Azam FC, Yakubu Mohammed, anatarajia kukaa nje ya dimba kwa muda wa wiki sita kuanzia sasa baada ya kufungwa plasta gumu ‘P.O.P’ kwenye mguu wake wa kulia.

Yakubu amefungwa P.O.P baada ya kuvunjika mfupa wa nyuma kwenye kifundo cha mguu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya KMC ambao Azam FC ilishinda mabao 3-1 na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Daktari wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa amesema beki huyo atakaa na plasta hilo gumu kwa muda wa wiki nne kabla ya kwenda kutolewa.

“Kwa muda wa wiki nne atakuwa na P.O.P na baada ya hapo atakapotolewa P.O.P ataanza programu ya kurejesha mwili kwenye hali ya kawaida (rehabilitation) kwa muda wa wiki mbili kwa hiyo kuanzia sasa kwa muda wa wiki sita hatutakuwa na Yakubu Mohammed,” alisema.