Usajili

MASAU BWIRE AMUOMBEA MSAMAHA MCHEZAJI WAKE ALIYEMJERUHI OKWI

Mara baada ya kutokea purukushani uwanjani ambapo ilimfanya mchezaji Mau Bofu kupewa kadi nyekundu na kutolewa nje katika mchezo dhidi ya Simba, kuna habari kuhusu kilichotokea.

Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire ambaye ni mkongwe katika cheo hicho, ameomba radhi kwa niaba ya mchezaji wake, Mau Bofu kwa tukio hilo akisema ni kweli alifanya makosa na anastahili kusamehewa.

Bwire amesema mchezo wa soka ni mchezo wa kugusana, sasa inapotokea mmoja amemgusa mwenzie mpaka amepitiliza au amezidi kiwango kinachotakiwa ni jambo la kawaida kuona adhabu ikitolewa kwa mhusika.

Ofisa huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu amesema kuwa Bofu hakuwa na nia ya kumuumiza Okwi na ndiyo maana ametambua kosa lake, hivyo anaomba msamaha kwa Wnasimba, wadau wa soka na kwa Okwi mwenyewe ambaye ndiye aliyejeruhiwa.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom, Bofu alimpiga kwa makusudi Okwi sehemu ya shingo na kusababisha mchezaji huyo kushindwa kuendelea na mchezo huku Bofu akitolewa nje kwa kadi nyekundu.

Simba ilishinda mabao 3-0 katika kipute hicho kilichopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.