Usajili

SERENGETI YAINGIA KUIKOMBOA LIGI YA WANAWAKE, YATOA UDHAMINI MNONO

Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana walisaini mkataba wa miaka mitatu wa kuidhamini Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) kupitia Bia ya Serengeti Lite.

Makubaliano hayo yamefikiwa na kusaini mkataba wenye thamani ya Sh milioni 450.

Ikumbukwe kuwa Kampuni ya Serengeti Breweries pia inaidhamini Taifa Stars kupitia bia ya Serengeti Premium Lager.

Mkurugenzi Mtendaji Serengeti, Hellen Weesie ameeleza kuwa wanaamini udhamini huo utatoa msukumo kwa timu zote nane zinazoshiriki katika Hatua ya Nane Bora katika msimu huu wa pili wa ligi hiyo.

Mkataba huo ulisainiwa mbele ya wanahabari ambapo alikuwepo Hellen Weesie pamoja na Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wanawake Tanzania (TWFA), Amina Karuma alisema udhamini huo wanaupokea kwa furaha kubwa kwa kuwa utasaidia kutimiza lengo kwa mpira wa Wanawake kuchezwa kwa ufanisi.