Usajili

OBREY CHIRWA AIRUDISHA YANGA DAR

Yanga imeshindwa kuendelea kuonyesha ubabe baada ya kuondolewa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kufungwa kwa penati na URA ya Uganda.

Yanga ambayo ilikuwa ikipewa nafasi ya kufanya kweli katika michuano hiyo kwa kufika fainali na ikiwezekana kitwaa ubingwa, imeishia hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani unguja dhidi ya wapinzani wao hao ambao pia waliiondoa Simba katika hatua ya makundi.

Hadi dakika za kawaida za mchezo zinakamilika matokeo yalikuwa suluhu ndipo ikabidi mchezo huo uamuliwe kwa kupigwa mikwaju ya penati.

Yanga ilipata penati nne huku wapinzani wao wakipata tano, mchezaji wa Yanga aliyekosa penati katika mchezo huo ni Obrey Chirwa ambaye ulikuwa ni mchezo wake wa kwanza kucheza baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda kutokana na madai yake ya kimaslahi dhidi ya uongozi wa klabu yake.

Kutokana na matokeo hayo, sasa URA imefanikiwa kufuzu hatua ya fainali ambayo itachezwa Jumamosi hii, ikisubiri matokeo ya Azam FC dhidi ya Singida United.