Usajili

KOCHA SIMBA ANAAMINI WATAFANYA KWELI, AFUNGUKA KUHUSU USAJILI WATAKAOFANYA

Kocha Msaidizi wa Simba, Masud Djuma, amesema wapo kwenye mchakato wa mwisho kutangaza majina ya wachezaji ambao wamekamilisha taratibu zao za usajili kwa ajili ya kuichezea timu yao ligi itakapo endelea.

Djuma amesema hawezi kutaja majina ya wachezaji hao kwa kuwa bado hawajamalizana nao na uongozi wa timu yao kwasasa unapambana kuhakikisha hilo linakamilika ndani ya wiki hii.

"Zoezi la usajili linakwenda vizuri na Kamati husika ya usajili inaendelea vizuri na kazi yake na mambo yakienda vizuri ndani ya wiki hii tuta watambulisha wachezaji wiwili ambao ni beki wa kati mmoja na kiungo mmoja," amesema Djuma ambaye amehudumu Simba akichukua nafasi ya Jackson Mayanja.

Kocha huyo aliyetua Simba, akitokea Rayon Sports ya Rwanda, amesema mipango yao ni kuongeza wachezaji wanne hivyo baada ya kutambulisha nyota hao wawili Kamati yao itaendelea na zoezi hilo kukamilisha wawili waliobaki ili kukiboresha kikosi chao ambacho kimeonekana kuwa na mapungufu katika baadhi ya nafasi.

Amesema anaamini kama wachezaji hao watapatikana kwa wakati na kupata muda wa kutosha kujiunga na wenzao haoni kama kuna timu inaweza kuisumbua Simba, kutokana na ubora wa timu waliyokuwa nayo msimu huu ambayo ilikosa vitu vichache ili kupata matokeo mazuri.

Wakati ligi imekwenda mapumziko mafupi kupisha michuano ya Kombe la Chalenji, inayoendelea nchini Kenya Simba ndiyo vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, wakiwa wamejikusanyia pointi 23, katika michezo 11 waliyocheza.