Wachezaji

Deus Kaseke

Deus Kaseke
Midfielder

 • Full Name

  Deus Kaseke

 • Date of Birth

  August 27th, 1994

 • Place of Birth

  Mbeya

 • Height

  165 cm

 • Weight

  70 kg

Career

 • Matches: 40
 • Goals: 6
 • Discipline: 3 fouls against
 • Passing: 23
 • Club Name: Young Africans Sports Club
 • Club Debut: March 24th, 2014
 • Previous Club: Mbeya City Council Football Club
Young Africans Sports Club 40 Matches Played

Overview

Kiungo wa Yanga ambaye alisajiliwa akitokea Mbeya City FC ya Mbeya. Kaseke alianza kupata umaarufu mkubwa akiichezea Mbeya City msimu wa 2013/2014 na msimu wa 2014/2015.

Deus Kaseke alianza kucheza mpira shule ya msingi, alikuwa akicheza kama kujifurahisha na hakuichukulia kuwa ni kazi rasmi. Alisoma katika Shule ya Sekondari Kalobe, kutokana na kipaji chake cha soka akachaguliwa kuwa waziri wa michezo shuleni hapo mwaka 2008.

Deus Kaseke amezaliwa 27 Agosti 1994. Alipohitimu akaendelea kucheza mtaani katika timu ya mtaani kwake Mbeya, Nzovye, timu hiyo inaitwa African Boys, baadaye alipata nafasi ya kuzichezea timu nyingine zikiwemo Simike FC na Airport Rangers.

Akiwa Airport kuna kaka yake anaitwa Venas Mligo alimfanyia mpango akajiunga na Mbaspo Academy (Mbeya).

Alipoona imetosha akaamua kutafuta timu Ligi Daraja la Kwanza, akaamua kwenda Prisons ambao hawakuvutiwa naye, ndipo akaamua kwenda Polisi Iringa ambapo alisajiliwa bure.

Kaseke aliwahi kunukuliwa akisimulia historia iliyofuata baada ya hapo, ambapo alisema: “Nilipofika Polisi Iringa nilisajili bure kabisa, nikaona mkataba na kusainii tu kwa sababu nilikuwa natafuta nafasi ya kutoka. Kuna kiongozi mmoja wa Polisi anaitwa Willy Chikweo, akaniambia mdogo wangu hapa umekuja kucheza, unasaini tu, sisi hatuna hela.

“Kwa sababu umekuja kucheza utatoka mwanangu. Nikamwambia hakuna tatizo, nikafanikiwa kucheza pale na nilikuwa nacheza namba sita kwa mechi zote saba, lakini hatukufanikiwa kwenda kwenye kituo cha Morogoro. Nikarudi Mbeya sina hata mia, wazazi wangu wakaniuliza sasa mpira unakusaidia nini mwanzetu?

“Unajua mimi nilikuwa nasoma chuo cha ualimu, sisi familia yetu ni kubwa, mzee wangu alikuwa ananilipia ada laki tano au sita, nikamwambia mzee niache, wasomeshe wadogo zangu, mimi nitapambana.

“Kitu kilichonifanya niache chuo ni Prisons. Waliniambia Deus utacheza hapa, njoo ufanye usaili, nikamwambia mzee mimi pale (Prisons) nitapata kazi, endelea kuwashughulikia wadogo zangu.

“Baba akaniacha na nikaenda Prisons, lakini sikusajiliwa na ndipo nikaenda Polisi Iringa na kucheza kwa nusu msimu kwa sababu nilienda raundi ya pili, lakini hatukufanikiwa kufika 9 Bora ambayo walienda Mbeya City na msimu huo waliopanda ligi kuu walikuwa Prisons, Polisi Moro na Mgambo katika kituo cha Morogoro.  

“Baada ya kupanda ligi kuu, Prisons wakasema lazima nikacheze pale, nikaenda kufanya usaili kwa mara ya pili, nilionekana kama napata nafasi, lakini wakasema utacheza timu ndogo. Nikawaambia haiwezekani bora waniache, nakumbuka kipindi kile Prisons waliwaacha wachezaji wengi walioipandisha timu.

KUELEKEA MBEYA CITY FC
Deus Kaseke anaeleza: “Kipindi Maka Mwalwisyi anakwenda kuwa kocha msaidizi pale Mbeya City, nikampigia simu mwalimu Mwambusi (Juma) nikimuonba nifanye majaribio. Mwalimu (Mwambusi) yeye alijua mimi nacheza namba sita, akaniambia Deus namba sita imejaa, nikamwambia mimi sichezi namba sita, nataka kucheza namba za mbele, akaniambia basi poa.

“Ikabidi nianze kufanya usaili, ilikuwa unafika uwanjani, unafanya ‘warm-up’ halafu mnaingia kucheza timu mbili. Bahati nzuri mimi nikacheza vizuri na kuonyesha naweza kucheza Mbeya City na kwenye usaili huo nilikuwa nacheza namba 10, 7 na 11.

“Baada ya kumaliza usaili, wakaniambia tutakupigia simu (Mbeya City), kweli Mwambusi akanipigia simu akiniambia Deus uje mazoezini kesho asubuhi, lakini sikujua kama nimechaguliwa kucheza Mbeya City.

“Nikaenda mazoezini kesho yake, nikaenda tena kesho yake,  akaniambia Deus utaingia kambini. Sikuamini kama kweli nimechaguliwa kucheza Mbeya City ya daraja la kwanza. Sikuchukua hela yoyote pia katika usajili, nilijua natafuta nafasi. Sasa kipindi tunapandisha timu ligi kuu, mimi niliibuka mfungaji bora wa Mbeya City nikifunga mabao manne.”

Msimu wa 2013/2014 Mbeya City ilikuwa tishio lakini msimu wa 2014/2015 ikapoteza makali. Kaseke anafafanua:

“Unajua msimu wa kwanza tulipofanya vizuri, watu wakaanza kutufikiria kivingine. Kila mtu anawaza kwamba akikutana na Mbeya City anakutana na timu bora, kwa kifupi hatukuwa na mpango B ‘Plan B’, tulicheza kwa staili ileile ya msimu uliopita.

“Upinzani ukawa mkubwa, watu wakawa wanajiandaa kuliko sisi tulivyo, sisi hatukubadilisha staili ya uchezaji, ilitupa wakati mgumu mechi saba za kwanza, tulipoteza mechi nne mfululizo, ligi iliposimama tukashukuru kwa sababu tuliona tunaweza kushuka daraja.

“Baada ya ligi kusimama tukajipanga vizuri, lakini wachezaji ambao walikuwa tegemeo kwenye timu wengi wakaachwa, tukaanza wakati wa mpito tena. Sikuelewa kwa nini wameachwa, sababu walikuwa nazo viongozi. Wachezaji tukaanza kuwaza kama wanaachwa wale ambao tulikuwa tunafanya nao kazi vizuri kama vile Saady Kipanga, Antony Matogolo (walitolewa kwa mkopo), Deogratius Julius (aliachwa), tutafanyeji? Lakini tukajua viongozi wanatafuta mchawi.

“Tungekuwa pamoja na wale wenzetu tungefanya vizuri kwa sababu tulikuwa tunajuana. Tulituliza akili baada ya kurudi tuliamini kwamba hatuwezi kushuka daraja, hata watu walikuwa wananiuliza ‘Deus mtashuka daraja? Nikawa nawaambia sisi tutashika nafasi nne za juu. Tulipofanikiwa nikawaambia mmeona?”

ALIWANIWA NA SIMBA
Deus Kaseke anasimulia: “Ujue tangu mwanzo waliokuwa wananifuatilia sana ni Simba. Nilikuwa nafanya nao mazungumzo tangu msimu wa kwanza, lakini hata Yanga walikuwa wananifuatilia, ila Simba walikuwa ‘serious’ zaidi na nikajua naenda kucheza Simba.

“Baada ya kupoteza mechi nne za kwanza msimu uliokwisha na ligi kusimama tulipofika raundi ya saba, Simba wakaniita huku Dar, tukafanya mazungumzo ya awali, wao walikuwa wananihitaji kwa kipindi hiki ambacho nimesaini Yanga. Wakaniambia nitasaini mkataba mwezi wa 12, halafu inapofika mwezi wa sita mwaka huu nitamalizia ada yangu ya usajili.

“Siku hiyo Yanga wakanitorosha usiku, nikaenda hoteli moja, waling’ang’ania nisaini kipindi kilekile, nikawaambia Yanga niacheni kwanza nitakuja kusaini mwishoni mwa msimu. Malengo yangu nilijua kufikia mwishoni mwa msimu mkataba wangu utakuwa umeisha, nilibishana nao (Yanga) mpaka wakamtuma kiongozi mmoja ambaye nilienda naye Mbeya, lakini nilipofika Mbeya nikaweka akilini mwangu kuwa kati ya timu hizi mbili (Simba na Yanga) lazima nitasaini timu moja.

“Baada ya kumaliza mkataba Mbeya City, Yanga wakawa serious kunitafuta, nikawa naongea na simu za Yanga tu. Simba wakanipigia simu wakiniambia hebu tutumie namba ya Peter Mwalyanzi, nikawatumia. Wao walitaka mimi na Peter twende Simba, kila nikipiga hesabu nikaona ngoja nitulie kwanza. Nakawaambia ngoja nimalize ligi, hata waandishi wa habari nilikuwa nawaambia mwenye kisu kikali ndiye atayekula nyama.”

SIKU YA KUSAINI YANGA
“Wakati natoka Mbeya nilijua naenda kusaini Yanga kwa sababu ndio walikuwa serious kwa siku mbili, tatu, napanda ndege Airport Mbeya napigiwa simu na viongozi wa Simba, Deus kumbe unakuja Dar? Unakuja kusaini Yanga?  Nikawaambia naenda kufanya nao mazungumzo, siendi kusaini.

“Nafika Airport Dar kumbe kuna viongozi wa Yanga wamekaa pale, wakati huohuo napigiwa simu na viongozi wa Simba wakiniuliza uko wapi? Sisi tumeshafika airport hapa? Nikawaambia naenda kufanya mazungumzo tu na Yanga, siendi kusaini.

“Usiku wake nilipata taabu sana usiku, kuna watu ambao mimi siwajui walitumwa na Simba waje kunichukua hotelini na kunipeleka sehemu fulani tumalizane. Yanga wakashitukia, ikabidi waje hotelini.  

“Mimi sikutaka kutoka pale hotelini kwa sababu hawakunileta wao, nikawaambia Simba ninyi ofa yenu mnasemaje? Mimi sijasaini Yanga.

“Ilipofika saa sita usiku wakaja viongozi wa Yanga hotelini, wakanipigia simu, nikawaambia mimi nalala, tutaongea kesho asubuhi. Mmoja wa viongozi wa Simba naye akanipigia simu akiniambia basi tutaongea kesho, lakini lazima tukuchukue hapo tukupeleke sehemu fulani.

“Kumbe viongozi wa Yanga wanajua hizo taarifa, wakaja chumbani kuniambia ofa yao, wakakaa kikao na kuniambania Deus hapa inabidi tuhame. Tukakaa pale mpaka saa saba kasoro, wakasema hawawezi kulala mpaka mimi na wao tuondoke.

“Nikahamishiwa hoteli moja pale Sinza inaitwa Golden Park, tulipofika pale bado simu za Simba zikawa zinapigwa, nikawaambia tutaongea kesho, nimelala, simu zikaendelea kupigwa, ikabidi nizime simu ili niweze kulala.

“Wakati nalala kumbe viongozi wa Yanga nao wamelala hotelini hapo, wanaogopa kwamba nitatoka. Sasa mimi naamka jamaa mmoja ananiambia, bwana Deus mimi nipo hapa tangu usiku, nimelala chumba hiki kinachotazamana na chako, nilishindwa kukwambia kwamba nimelala hapa, nilitaka jamaa (Simba) wasifanikiwe kukutoa.

“Lakini nilipokuwa nakuja Dar kusaini, watu wanaonisimamia waliniambia mwalimu Pluijm (Hans van der wa Yanga) ndiye aliyenipendekeza mimi kwamba “namhitaji Deus”. Nikawa najiuliza nitaendaje Simba wakati mwalimu ndio huyo anaondoka?  Nikienda Azam si ndiyo hao wanahangaika kutafuta kocha?

“Azam nao walinipigia simu lakini hawakuwa serious. Nilipofika hapa Dar si unajua Watanzania tena, wakawa wanapandisha mzigo washindana wao kwa wao. Ikabidi niwaambie Yanga tukifika hapa (dau) hata aje nani sitasaini kokote. Wakafika dau nikasaini Young Africans miaka miwili.”

SABABU YA JEZI NAMBA 4
Kaseke aliwahi kusema kuwa alikuwa akivutiwa na kiungo wa zamani wa Yanga, Athumani Idd ‘Chuji’ ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitumia jezi namba 4.

Chuji ambaye alicheza Yanga kwa mafanikio makubwa ni mchezaji kipenzi cha Kaseke, hivyo aliamua kutumia jezi kama yake (namba 4) akiamini siku moja atafanikiwa kama nyota huyo.