Timu

Twiga Stars

Twiga Stars national

 • Established in

  2002

 • Club President

  Haruna Niyonzima

 • Manager Name

  George Lwandamina

 • Location

  Dar es Salaam

CLUB HISTORY

 

Twiga Stars ilianzishwa mwaka 2002. Hicho kilikuwa ni kipindi cha uongozi wa kilichokuwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) sasa TFF- Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania chini ya uenyekiti wa Muhidin Ndolanga na Katibu Mkuu Michael Wambura.

Timu hiyo ililazimika kuundwa haraka haraka baada ya uongozi wa FAT chini ya Ndolanga na Katibu Mkuu wake Ismail Aden Rage kuthibitisha kushiriki mashindano ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kwa fainali za mwaka 2002. Uthibitisho huo ulifanywa Novemba mwaka 2001.

Ikumbukwe kuwa Desemba 2001 ulifanyika uchaguzi wa FAT jijini Arusha ambapo Rage alishindwa kutetea kiti chake baada ya kushindwa na Wambura. Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda katika uchaguzi huo ni Kanali Idd Kipingu (Makamu Mwenyekiti) na Charles Masanja (Katibu Msaidizi).

Wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji ni Adam Brown, Amani Komanya, Amin Bakhresa, Amir Roshan, Bakari Makanjira, Festo Mkemwa, Joseph Mapunda, Jumbe Magati, Method Buberwa na Subira Mambo.

Rage naye aliingia madarakani mwaka 1996 baada ya kumshinda Kanali Ali Mwanakatwe katika uchaguzi uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ndolanga kwa upande wake alifanikiwa kutetea wadhifa wake katika uchaguzi wa 1993 mjini Kibaha, 1996 na 2001 kabla ya kuanguka kwenye uchaguzi wa Desemba 2004.

Kwa vile FAT ilishathibitisha kushiriki AWC, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilitangaza ratiba ya mechi za hatua ya awali ikiwemo Tanzania dhidi ya Eritrea. Hali hiyo iliifanya FAT chini ya Mtendaji mpya (Wambura) kulazimika kuunda haraka haraka Twiga Stars.

Haikuwa rahisi kufanya hivyo, kwani wakati huo hakukuwa na ligi inayoeleweka ambapo mpira wa miguu wa wanawake ulikuwa ukichezwa zaidi wilayani Kinondoni, Dar es Salaam pekee.

Hata hivyo, FAT ililazimika kuigeuza timu ya Sayari Women ambayo ilikuwa maarufu Kinondoni na Tanzania kwa ujumla kwa mpira wa miguu wa wanawake kuwa timu ya Taifa. Hiyo ilikuwa rahisi kwa vile wakati huo Sayari ndiyo ilikuwa imetoka Denmark ambapo ilikuwa na mialiko ya karibu kila mwaka kwenda huko kwenye mashindano.

Baadhi ya wachezaji waliounda Twiga Stars wakati huo ni Esther Chabruma, Mwaka Kaveva, Mwanaidi Yusuf, Hija John, Mwapewa Mtumwa, Sweet Paul, Khadija Makwega, Tatu Omari, Masha Ali, Mosi Juma, Dogo Seif, Tabu Rajab, Habiba Said, Monica Mathew, Esther Paul na makipa Salama Machupa na

Mwanaisha Ali. Mwapewa amerudi katika timu hiyo baada ya kutokuwepo kwa muda mrefu.

Kocha wa kwanza wa Twiga Stars alikuwa Juma Bomba ambaye pia alikuwa akiinoa Sayari Women. Baada ya kurejea kutoka Eritrea kwenye mechi ya kwanza ndipo Idd Machupa (Katibu Mkuu wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu -TAFCA wakati huo) akateuliwa kuwa Kocha Mkuu, na Bomba akibaki kuwa msaidizi.

AWC ilianza mwaka 1998 nchini Nigeria ambapo wenyeji walikuwa mabingwa. Nigeria ndiyo imekuwa ikitamba katika mashindano hayo kwa kunyakua ubingwa mara tano (1998, 2000 nchini Afrika Kusini, 2004 nchini Afrika Kusini, 2006 nchini Nigeria na 2010 nchini Afrika Kusini).

Nchi nyingine ambazo zimewahi kutwaa ubingwa ni Cameroon mwaka 2002 nchini Nigeria, na Equatorial Guinea mwaka 2008 nchini mwao. Afrika Kusini ndiyo nchi iliyoandaa fainali nyingi bila kutwaa ubingwa. Iliandaa fainali za AWC mwaka 2000, 2004 na 2010.

Twiga Stars ilifuzu kwa mara ya kwanza fainali za AWC zilizofanyika 2010 nchini Afrika Kusini. Kufikia huko katika raundi ya awali iliitoa Ethiopia kwa jumla ya mabao 4-2. Ilishinda mechi ya kwanza ugenini mabao 3-1 kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani.

Katika raundi ya kwanza iliitandika Eritrea kwa jumla ya mabao 11-4. Twiga Stars ilishinda nyumbani mabao 8-1 na kutoka sare ya mabao 3-3 jijini Asmara, hivyo kupata tiketi ya kwenda kwenye fainali Afrika Kusini.

Ikiwa katika kundi A katika fainali nchini Afrika Kusini, Twiga Stars ilipoteza mechi zote tatu. Ilishika mkia katika kundi hilo ambalo vinara wake walikuwa Nigeria. Mechi ya kwanza ilifungwa na wenyeji Afrika Kusini mabao 2-1 huku bao lake likifungwa dakika ya 43 na Esther Chabruma.

Ilishindwa kufua dafu mbele ya Mali katika mechi iliyofuata kwa kufungwa mabao 3-2. Mabao ya Twiga Stars yalifungwa na nahodha Sophia Mwasikili dakika ya 30 na Fatuma Mustafa akifunga lingine dakika ya 32. Mechi ya mwisho hatua ya makundi ilifungwa 3-0 na Nigeria.

Baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye fainali za Afrika Kusini mwaka juzi ni Fatuma Omari, Fatuma Bashiri, Mwajuma Abdallah, Sophia Mwasikili, Mwanahamisi Omari, Asha Rashid, Etoe Mlenzi, Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa, Pulkeria Charaji, Hellen Peter, Mwanaidi Tamba, Maimuna Said na Esther Chabruma.

Twiga Stars ambayo hivi sasa ni moja ya timu nane bora za Afrika iko katika kampeni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za AWC ambazo zitafanyika jijini Malabo, Equatorial Guinea mwezi Novemba mwaka huu.

Katika raundi ya mchujo inapambana na Namibia ambapo ilishinda mechi ya kwanza ugenini Januari 21 mwaka huu kwa mabao ya Asha Rashid na Mwanahamisi Omari. Timu hizo zinarudiana Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Ikiitoa Namibia itacheza na mshindi kati ya Misri na Ethiopia. Ikivuka hapo itakwenda kwenye fainali nchini Equatorial Guinea ambayo inashirikisha nchi nane ikiwemo mwenyeji Equatorial Guinea.

Mwaka jana Twiga Stars ilishiriki mashindano ya wanawake ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) yaliyofanyika Julai jijini Harare na kushika nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa Zimbabwe na makamu bingwa Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’.

Katika michuano hiyo ilizifunga Botswana 3-1, Zambia 2-0 na kufungwa 1-0 na Afrika Kusini. Ilipoteza mechi ya nusu fainali dhidi ya Zimbabwe kwa penalti 4-2. Penalti zake zilifungwa na Sophia Mwasikili na Mwanahamisi Omari. Ilishinda mechi ya kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Malawi kwa mabao 3-2. Asha Rashid alifunga mawili, na lingine likifungwa na Mwanahamisi Omari.

Pia Septemba mwaka jana, Twiga Stars ilishiriki michezo ya All Africa Games (AAG) iliyofanyika jijini Maputo, Msumbiji. Ilipoteza mechi ya kwanza kwa kufungwa mabao 2-1 na Ghana. Bao la Twiga Stars lilifungwa na Mwanahamisi Omari.

Mechi iliyofuata ilitoka sare ya mabao 2-2 na Afrika Kusini huku wafungaji wake wakiwa Mwanahamisi Omari na Zena Khamis. Mechi ya mwisho pia walitoka sare ya mabao 2-2 na Zimbabwe. Wafungaji wa Twiga Stars walikuwa Asha Rashid and Mwanahamisi Omari.

Mwanahamisi Omari ndiye nyota wa ufungaji katika timu hiyo ambapo amekuwa akifunga karibu katika kila mechi ambayo Twiga Stars inacheza, iwe imeshinda au imeshindwa.

Wachezaji wa sasa wanaounda kikosi cha Twiga Stars na klabu zao kwenye mabano ni Sophia Mwasikili (Sayari Women), Fatuma Bushiri (Simba Queens), Fatuma Omari (Sayari Women), Mwajuma Abdallah (JKT), Asha Rashid (Mburahati Queens), Mwanahamisi Omari (Mburahati Queens), Etoe Mlenzi (JKT), Zena Khamis (Mburahati Queens), Fatuma Khatib (Mburahati Queens), Maimuna Said (JKT), Fadhila Hamad (Uzuri Queens), Fatuma Mustafa (Sayari Women) na Evelyn Senkubo (Mburahati Queens).

Wengine ni Rukia Hamisi (Sayari Women), Mwapewa Mtumwa (Evergreen), Judith Hassan (TMK), Aziza Mwadini (Zanzibar), Sabai Yusuf (Zanzibar), Semeni Abeid (Tanzanite Queens), Zena Said (Uzuri Queens), Pulkeria Charaji (Sayari Women), Tatu Said (Makongo Sekondari), Mwanaidi Hamisi (Uzuri Queens), Hanifa Idd (Uzuri Queens) na Fatuma Gotagota (Mburahati Queens).

Mbali ya Bomba, Machupa na kocha wa sasa Charles Boniface Mkwasa, Twiga Stars pia imewahi kufundishwa na kocha Selemani Gwaje.

Mafanikio ambayo Twiga Stars imepata, hasa kwa kucheza fainali za AWC yanatoa mwanga mpya wa mpira wa miguu wa wanawake nchini. Ni wazi mafanikio ya haraka kwa Tanzania kimataifa yanaweza kupatikana kupitia timu hiyo kwani ina uwezo na ushindani kwa mpira wa miguu wa wanawake bado si mkubwa kulinganisha na ule wa mpira wa miguu kwa wanaume.

Imeandaliwa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura

 

Qualifying African Women Championship 2010, South Africa

2010