Habari za Kitaifa

REFA MBEYA CITY VS SIMBA ATOKA UWANJANI AKIWA NDANI YA KARANDINGA

Muda mfupi baada ya Simba kufanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom, kulitokea hali ya sintofahamu kuhusu waamuzi wa mchezo huo.

Mara baada ya kipenga cha mwisho katika kipute hicho kwenye Uwanja wa Kumbukukumbu Sokoine mkoani Mbeya, waamuzi wa mchezo huo walilazimika kuondoka uwanjani hapo wakiwa ndani ya karandinga la polisi kutokana na usalama wao kuonekana kuwa mdogo.

Waamuzi hao walichukua hatua hiyo kutokana na kile kilichoonekana walitaka kufanyiwa fujo na baadhi ya mashabiki wa Mbeya City waliokuwa na dhana kuwa timu yao haijatendewa haki.

Mchezo wa jana ulichezeshwa na refa Ahmed Kikumbo aliyesaidiwa na Omari Juma wote wa Dodoma na Michael Mkongwa kutoka Njombe, Simba ilipata bao hilo kipindi cha kwanza, likifungwa na winga, Shiza Ramadhani Kichuya. 

Kichuya alifunga bao hilo dakika ya saba baada ya mabeki wa Mbeya City kusita kumdhibiti wakidhani ameotea kufuatia pasi ndefu ya juu ya kiungo Jonas Mkude. 

Ushindi huo unaifanya Simba ifikishe pointi 19 baada ya kucheza mechi tisa na kupanda kileleni ikiizidi kwa wastani wa mabao tu Azam yenye pointi 19 pia.