Habari za Kitaifa

RAIS MAGUFULI AKUBALI KUIKABIDHI SIMBA KOMBE JUMAMOSI

Baada ya uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kwa rais wake, Wallace Karia kutuma maombi kwa Waziri wa Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kuomba Rais wa Jamhuri ya Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akabidhi kombe la VPL kwa Simba ambao ndiyo mabingwa wa msimu huu 2017/18, maombi hayo yamekubaliwa.

Simba itakabidhiwa kombe hilo siku ya Jumamosi Mei 19, 2018 baada ya mchezo wao wa mwisho wa ligi kwenye Uwanja wa Taifa) dhidi ya Kagera Sugar.

TFF imetangaza kuwa maombi hayo yamekubaliwa na Rais Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika mchezo huo.

Aidha, Rais Magufuli atakabidhiwa Kombe la CECAFA U17 Championship na timu ya vijana ya U17 ‘Serengeti Boys’ baada ya timu hiyo kushinda kombe hilo Aprili 29, 2018 nchini Burundi.