Habari za Kitaifa

BAADA YA KUCHEMKA UWANJANI, STRAIKA MGHANA AONDOKA AZAM

Straika Mghana wa Azam FC, Bernard Arthur amevunja mkataba na klabu yake hiyo iliyomsajili kwenye dirisha dogo msimu huu.

Imeelezwa kuwa Arthur aliyesajiliwa na matajiri hao wa Lambalamba kutoka Liberty Professionals ya Ghana, amemalizana na Azam baada ya kushindwa kuitumikia kikamilifu timu hiyo  iliyokuwa chini ya Kocha Mromania Cioaba Aristica. 

Kuondoka kwa Arthur  mwenye miaka 21 ni muendelezo wa sehemu ya watu wanaoondolewa kikosini hapo,  ambao ni pamoja na kocha huyo raia wa Romania na Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdul Mohamed ambaye amebadilishiwa madaraka.

Hata hivyo, juhudi za kuwapata viongozi wa Azam na Arthur watolee ufafanuzi  juu ya suala hilo ziligonga mwamba kwani simu zao ziliita bila mafanikio.