Habari za Kitaifa

OKWI ANAITAFUTA REKODI YA MOHAMMED HUSSEIN ‘MMACHINGA’

 

Licha ya kuwa mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi anaongoza kwa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom lakini bado ana kibarua kigumu cha kusaka mabao ili kuvunja rekodi ya mabao 26 iliyodumu kwa miaka 19 ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.

Wakati Simba ikiingia uwanjani kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya Prisons ili kusogelea ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Okwi atakuwa na changamoto nyingine ya kuhakikisha anafunga mabao ya kutosha ili ajitengenezee mazingira mazuri ya kuvunja rekodi iliyowashinda washambuliaji wenzake kwa miaka 19.

Mmachinga amemtabiria Okwi kuvunja rekodi hiyo msimu huu akisema ni mshambuliaji mzuri mwenye uchu wa mabao hivyo ana nafasi ya kuyafikia mabao yake.

Okwi mwenye mabao 18 ameifikia rekodi ya Boniface Ambani wa Yanga aliyefunga mabao 18 msimu wa 2008/2009, Mussa Hassan Mgosi (Simba) aliyefunga mabao 18 msimu wa 2009/2010 na Mrisho Ngassa (Yanga) aliyefunga mabao 18 msimu wa 2010/2011.