Habari za Kitaifa

KINA KASEJA UWANJANI LEO, WAPIGWA MKWARA NA MWADUI FC

Kikosi cha Mwadui FC kinatarajiwa kucheza dhidi Kagera Sugar katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, leo Jumanne.

Kuelekea mchezo huo Mwadui FC imetamba kuwa inahitaji ushindi na haitakuwa tayari kupoteza pointi tatu kirahisi.

Katika mchezo wao uliopita, Mwadui FC ilipata kipigo cha bao 1-0, wakati Kagera Sugar yenyewe ikipata kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Yanga.

Mpaka sasa Kagera ambayo inatarajiwa kuongozwa na kipa Juma Kaseja imekusanya pointi 18 ikiwa nafasi ya 14, huku Mwadui ikiwa na alama 20 katika nafasi ya 12 kila moja ikicheza mechi 21 na Mwadui walisisitiza wanazitaka pointi tatu ili kujiondoa katika eneo la hatari ya kushuka daraja.

Ally Bizimungu ambaye ni Kocha wa Mwadui, amesema amekiandaa vyema kikosi chake ili kupata ushindi, lakini hata kwa mechi nyingine anataka kushinda zote.

Alisema kikosi chake hakipo sehemu nzuri, hivyo ushindi wa leo ni muhimu katika vita ya kupambana kujinasua kutoka chini na kusema kuwa, wataingia uwanjani kwa tahadhari na umakini wa hali ya juu.

Katika mchezo huo, Mwadui FC itawakosa viungo wake Abdallah Seseme na Awesu Awesu ambao ni majeruhi, ambapo Bizimungu atalazimika kufanya mabadiliko.