Habari za Kitaifa

KIPIGO CHA YANGA CHAMVURUGA KOCHA WA STAND UNITED, ALALAMIKIA WAAMUZI

Baada ya kushuhudia timu yake ikipata kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Yanga, Kocha Msaidizi wa Stand United, Athumani Bilali ‘Billo’ amedai kuwa wapinzani wao walibeba katika mchezo huo.

Bilo ambaye ni mwenyeji wa Mwanza amesema kuwa waamuzi waliochezesha mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacon, jana Jumatatu hawakuwatendea haki wao kwa kuwa walifanya makosa ambayo yaliigharimu timu yake na kusababisha kupoteza mchezo.

Ikumbukwe kuwa wiki moja iliyopiuta Stand iliikomalia Simba na mchezo wao kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo ndipo kulipofanyika mchezo huo wa jana.

Billo amelalamikia kitendo cha mwamuzi wa pembeni kuonyesha mfungaji wa bao la kwanza la Yanga aliotea lakini baadaye akashusha kibendera.

“Tumepoteza mchezo kwa nguvu za waamuzi kwa sababu waliisaidia timu pinzani kwa makosa madogomadogo ya hapa na pale, goli la kwanza wakati linafungwa line one ananyoosha kibendera wachezaji wangu wakasimama Yanga wakafunga.

“Waamuzi waliochezesha mchezo wetu dhidi ya Yanga mimi binafsi sijawafurahia.”

Kuhusu safu yake ya ushambuliaji kupoteza nafasi nyingi za kufunga mabao, Billo amesema ni kukukosa umakini lakini tatizo hilo litashughulikiwa na benchi la ufundi.

“Ni umakini mdogo wa washambuliaji wetu kwa sababu tumetengeneza nafasi saba tumefunga moja kwa hiyo hilo suala tutalifanyia kazi nadhani mechi ijayo tutafanya vizuri.”