Habari za Kitaifa

MSAFARA WA AZAM FC WAPOKEWA KWA MBWEMBWE DAR ES SALAAM

 

Baada ya kumaliza kazi kisiwani Unguja, kikosi cha Azam FC kimewasili jijini Dar es Salaam, asubuhi ya leo na kupokelewa na mashabiki wengi wa timu hiyo.

Azam FC imetwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa mara ya pili mfululizo baada ya ushindi wa penati 4-3 dhidi ya URA ya Uganda kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa jana kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Fainali hiyo ilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, ambapo shujaa wa Azam FC alikuwa ni kipa, Mghana Razack Abalora aliyepangua mikwaju miwili ya URA.

Katika bandari ya Dar, wachezaji, viongozi na benchi la ufundi la Azam FC walionekana kuwa na furaha huku kukiwa na shangwe nyingi kutoka kwa mashabiki ambao baadhi yao walikuwa wamevaa jezi za timu hiyo na kushangilia kwa nguvu.