Habari za Kitaifa

BAADA YA UBINGWA WA MAPINDUZI CUP, AZAM FC IMECHUKUA MAAMUZI HAYA KUHUSU SURE BOY…

 

Azam Fc imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, hiyo ni baada ya kuifunga URA ya Uganda kwa penati 4-3.

Awali katika dakika 90 za mchezo huo, timu hizozilitoka suluhu ya 0-0 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, jana usiku kisiwani Unguja.

Baada ya kukabidhiwa ubingwa huo, taarifa kutoka Azam FC zinaeleza kuwa ubingwa huo wameutoa zawadi kwa kiungo wa timu hiyo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, na hii ni baada ya kufiwa na Mama yake mzazi wiki iliyopita wakati akiwa na timu hiyo kwenye harakati za kuwania taji hilo.

Hadi Azam FC inatwaa ubingwa, imeweza kucheza jumla ya mechi sita, ikishinda mara tano na kupoteza mmoja huku ikiruhusu nyavu zake kuguswa mara moja tu, na hii ni walipofungwa bao 1-0 dhidi ya URA kabla ya kulipa kisasi kwenye mchezo huo wa fainali.

Kikosi hicho kilitarajiwa kuondoka visiwani Zanzibar, asubuhi ya leo Jumapili kurejea jijini Dar es Salaam tayari kabisa kuanza maandalizi ya kuwakabili Majimaji ya Songea na Tanzania Prisons ya Mbeya, katika mechi zijazo mbili za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) zitakazofanyika wiki ijayo.