Habari za Kitaifa

AZAM FC YABEBA UBINGWA WA KOMBE LA MAPINDUZI, YAWEKA REKODI MPYA

Wakati ikitwaa taji la Kombe la Mapinduzi kwa mara ya pili mfululizo usiku wa jana, Azam FC imeandika rekodi mpya kwenye michuano hiyo baada ya kuwa ndiyo timu iliyolitwaa mara nyingi.

Mabingwa hao wamelitwaa taji hilo mara nne sasa, mara ya kwanza ililitwaa mwaka 2012 na kulibeba tena 2013 kabla ya kulichukua tena mara mbili mfululizo mwaka jana na huu.

Azam FC imetwaa taji hilo baada ya kuichapa URA ya Uganda kwa mikwaju ya penalti 4-3 kwenye mchezo wa fainali kufuatia dakika 90 kumalizika kwa suluhu.

Shujaa wa Azam FC alikuwa ni kipa Razak Abalora, aliyeokoa kiustadi penalti mbili za wachezaji wa URA, ya kwanza iliyopigwa na Patrick Mbowa na ile ya tano waliyopiga Brian Majwega huku nahodha msaidizi wa matajiri hao, Agrey Moris akifunga ya mwisho iliyoipa ubingwa timu hiyo.

Wachezaji wengine wa Azam FC waliopata mikwaju ya penalti ni nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Yakubu Mohammed na winga Enock Atta huku beki wa kushoto, Bruce Kangwa akikosa penalti pekee kwa upande wa mabingwa hao kutoka viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Ubingwa huo unaifanya Azam FC kutwaa taji la kwanza msimu huu, huku ikiwa inaongoza kwa kulitwaa ikifanya hivyo mara nne, ikifuatiwa na Simba iliyolibeba mara tatu.

Kama Azam FC ingekuwa makini basi huenda isingefika kwenye hatua ya changamoto ya mikwaju ya penalti hii ni kutokana na mshambuliaji wake, Bernard Arthur kushindwa kuzitumia vema nafasi tatu za wazi alizopata kipindi cha kwanza.

Mchezo huo uliokuwa mkali na wa aina yake uliohudhuriwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyekuwa mgeni rasmi, ulishuhudiwa kipa wa Azam FC, Abalora, akifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo mikali ya URA na kupelekea kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mechi hiyo.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:

Razak Abalora, Himid Mao (C), Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohammed, Abdallah Kheri/Joseph Mahundi dk 59, Stephan Kingue, Frank Domayo/Iddi Kipagwile dk 58, Salmin Hoza, Bernard Arthur/Shaaban Idd dk 58, Yahya Zayd/Enock Atta dk 64.