Habari za Kitaifa

VIFO VYA WACHEZAJI WA ZAMANI NI FUNZO KWA WACHEZAJI WA SASA

Baada ya wimbi kubwa la wachezaji wa zamani kufariki Dunia na kuzuka maneno mengi,kuonekana hawana lolote katika jamii na kutokuwa na uwezo wa kifedha, mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza Khalid Bitebo Zembwera amesema vifo hivyo  ni elimu tosha kwa wachezaji wa sasa kuhakikisha wanatumia fedha zao vizuri na kuweka akiba uzeeni ili wasije kuonaneka wa ajabu mbeleni.


"Hakika hili ni funzo kwa wachezaji wa sasa ambao wapo katika viwango vizuri na wanaopata stahiki zao za kutosha kuhakikisha wanatumia fedha zao vizuri ili kuweka akiba itakayo wasaidia baada ya Mpira"

 

Pia Bitebo akazungumzia kuhusiana na maisha ya soka kipindi cha zamani huku akisema wao walicheza kipindi ambacho hakukua na mambo mengi kama sasa na walikua wakilipwa kidogo sana, hali ambayo hata wangeweka akiba wasingefikia malengo yao kutokana na kukosa utamaduni wa  kuweka fedha.
"Sisi tulipambana sana zamani japokua hakukua na malipo mazuri kama hivi sasa na kutufanya tuishi maisha ya misaada kwa wale waliokua wanaburudika na soka letu kama zawadi ya upambanaji wetu."

 

Aidha Bitebo akaongezea kwa kusema amepokea kwa masikitiko vifo vya wachezaji wa  zamani wa soka la Tanzania, Mwamba Kapera na Athumani Juma Chama Jogoo ambaye aliwahi kucheza nae Pamba Sc miaka ya themanini huku akihuzunishwa na baadhi ya wapenda soka hapa nchini kuanza kuzungumzia maswala ya maisha bila kujua kua kuna muda lazima waelewe matatizo ya soka la Zamani.

Pia Bitebo akashauri kwa wachezaji hao wa zamani kuunda Chama chao na taasisi ambazo zitwasaidia baadae na kuepuka na mambo ya kufariki kwa kukosa fedha za matibabu huku akiwaomba wadau na wapenzi wa soka kuwakumbuka wachezaji wa zamani hasa katika mambo muhimu kama kuwepo katika vitengo mbalimbali kwenye soka la Tanzania.