Habari za Kitaifa

KOCHA LWANDAMINA AMTETEA OBREY CHIRWA

Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina amemtetea mshambuliaji wa timu yake, Obrey Chirwa, kwa kusema kuwa mkwaju wa penati aliokosa ilikuwa na bahati mbaya na hakufanya makusudi kama mashabiki wanavyodai.

Lwandamina ambaye hakuwepo katika kikosi hicho kwa wiki kadhaa kutokana na matatizo ya kifamilia amesema vitu kama hivyo, hutokea kwa mchezaji mwenye uwezo wa kupiga penati kama Chirwa hivyo haoni sababu ya mashabiki kumlaumu kwasababu hakukusudia.

Akifafanua zaidi alisema: "Hatupaswi kumpa lawama kwa sababu siku nyingine anaweza kukataa kufanya hivyo, na vitu kama hivyo ni kawaida kutokea kwa mchezaji mwenye kiwango kama cha Chirwa,” amesema Lwandamina.

Kocha huyo amesema ni wakati sasa wa kujipanga na kuangalia michuano inayowakabili mbele yao kuliko kubaki kumtupia lawama mchezaji kwa michuano ya wiki mbili ambayo nikama mazoezi.

Mara baada ya kukoa penati katika mchezo dhidi ya URA, mashabiki wengi wa timu yake walimshushia lawama Chirwa na kuonekana kama amefanya makusudi hasa ikizingatiwa kuwa hakuwepo kikosini hapo kwa wiki kadhaa kutokana na mgogoro wa kimaslahi kati yake na uongozi wa Yanga.