Habari za Kitaifa

SIMBA WAPIGWA MKWARA MZITO, TIMU YA MZUNGU YACHARUKA

Na Buddah Mtanzania, Mwanza

Baada ya kutolewa katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya mabingwa watetezi Azam FC, Singida United imeingia Dar es Salaam kwa lengo la kuweka kambi jijini hapo kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Simba unaotarajiwa kupigwa Januari 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na ShutiKali, Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga alisema wamepokea matokeo ya mchezo wao wa Kombe la Mapinduzi katika hatua ya Nusu Fainali dhidi ya Azam FC kwa mikono miwili na kinachofuata sasa ni kujipanga.

"Tumepokea matokeo kwa masikitiko lakini ndiyo hali ya mashindano ilivyo, sasa tumeshaingia Dar na tutaweka kambi mpaka siku ya mchezo wetu dhidi ya Simba."

Aidha, Sanga ambaye timu yake inanolewa na Kocha Hans van Pluijm raia wa Uholanzi, amemzungumzia mshambuliaji wao, Danny Usengimana aliyepata majeraha ya kuvunjika mkono kwenye mchezo dhidi ya Taifa Jang’ombe kuwa ameshapewa ruhusa kwenda nchini kwao, Rwanda kwa ajili ya kujiuguza majeraha hayo na kupata muda wa kupumzika.

Mchezo huo utazikutanisha Simba ikiwa inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku Singida United ikiwa katika nafasi ya tatu ikijikusanyia jumla ya alama 23 nyuma ya Azam FC na Simba zilizopo juu ya.

Ikiwa Singida United itashinda itapanda kwenye kilele cha ligi hiyo nyuma ya Yanga.