Habari za Kimataifa

REAL MADRIDI WACHUKUA KWA MARA YA TATU TAJI LA KLABU BINGWA ULAYA,YAILAZA LIVERPOOL GOLI 3 KWA 1

REAL MADRID wametawazwa kuwa mabingwa wa kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya baada ya kuwafunga Liverpool magoli matatu kwa moja na kuweka rekodi barani ulaya kwa kuchukua taji hilo mara tatu mfululizo taji ambalo linaifanya Real Madrid kutimiza jumla ya mataji 13 kwenye ligi ya mabingwa barani ulaya.

Liverpool ilipata pigo mapema tu katika mchezo wa leo, baada ya mshambuliaji wake nyota, Mmisri Mohammed Salah kutolewa nje dakika ya 30 kufuatia kuumia baada ya kugongana na beki na Nahodha wa Real Madrid, Sergio Ramos. 

Kipa Karius akawazawadia bao la kuongoza Real Madrid baada ya Karim Benzema kumpiga mpira bila uangalifu mbele ya Mfaransa huyo ukamgonga na kuingia nyavuni dakika ya 51. Mshambuliaji Msenegali, Sadio Mane akaisawazishia Liverpool dakika nne baadaye, kabla ya Gareth Bale kutokea benchi na kufunga mabao mawili dakika za 64 na 83. 

Karius aliwasili Liverpool akitokea Mainz mwaka 2016 na alikuwa na mwanzo mgumu kabla ya kuzinduka na kuwa kipa chaguo la kwanza mbele ya kocha Jurgen Klopp akimpindua kipa Simon Mignolet. Lakini makosa ya leo ya Karius hayatasahaulika milele.