Habari za Kimataifa

MSUVA AFANYA KWELI TENA MOROCCO, ATUPIA MABAO MAWILI

Simon Msuva ameendelea kuwa na kiwango kizuri  katika maisha yake ya soka nchini Morocco, hiyo ni baada ya kucheka na nyavu mara mbili akiitumikia timu yake ya Difaa Hassan El Jadida ilipokuwa ugenini kucheza dhidi ya Olympique de Khouribga.

Mabao hayo ya Msuva yalikuwa msaada kwa timu yake kufanikisha kupata sare ya mabao 3-3 ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu ya Morocco kwenye Uwanja wa Phosphate mjini Khouribga.

Matokeo hayo yanaiongezea pointi moja Jadida na kushuka kwa nafasi moja hadi ya nne kwenye Ligi ya Morocco yenye timu 16, ikifikisha pointi zake 38 baada ya kucheza mechi 25.

Msuva alitupia mabao hayo katika dakika za 65 na dakika ya 90, bao lingine la timu hiyo lilifungwa na Tarik Astati dakika ya 33.

Mabao ya Khouribga yamefungwa na Zouhair El Moutaraji mawili dakika za nne na 38 na Adam Nafati dakika ya 55.

Kikosi cha Difaa Hassan El-Jadida kilikuwa; Aziz El Qinani, Fabrice Ngah, Youssef Aguerdoum, Tarik Astati, Mohamed Hamami, Bakary N'diaye, Marouane Hadhoudi, Bilal El Magri, Saimon Msuva, Ayoub Nanah na Mario Mandrault Bernard