Habari za Kimataifa

TIMU YA MBWANA SAMATTA YATINGA FAINALI UBELGIJI

Mshambuliaji Mbwana Ally Samatta amekuwa mmoja wachezaji walioisaidia timu yake ya KRC Genk kupata ushindi wa bao 1-0 na kuingia fainali ya Kombe la Ubelgiji.

Genk imeifunga Kortrijk katika mchezo wa marudiano wa Nusu Fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.

Kwa matokeo hayo, Genk inasonga mbele kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya 3-3 kufuatia awali kufungwa 3-2 kwenye mchezo kwanza Uwanja wa Guldensporen mjini Kortrijk.

Mfungaji wa bao pekee la Genk usiku wa jana ni kiungo Msenegali mwenye umri wa miaka 28, Ibrahima Seck aliyefunga dakika ya 15 akimalizia pasi ya kiungo Mspaniola, Alejandro Pozuelo Melero.

Sasa, Genk itakutana na mshindi wa jumla kati ya Club Brugge na Standard Liege zinazotarajiwa kukutana leo, mechi ya kwanza Standard Liege ilishinda kwa mabao 4-1.