Habari za Kimataifa

MESSI, SUAREZ WAONGOZA JESHI LA BARCELONA KUSHINDA 5-0 KOMBE LA MFALME

 

Baada ya mchezo wa kwanza wa Kombe la Mfalme kati ya Barcelona dhidi ya Celta Vigo kumalizika kwa sare ya bao 1-1, safari hii Barcelona wakaweka utani pembeni na kuingiza jeshi kamili ambalo limetoe dozi ya mabao 5-0.

Katika mchezo huo wa kwanza wa Hatua ya 16 Bora ya kombe hilo la nchini Hispania, Barcelona ilichezesha kikosi cha pili kwa asilimia kubwa ambapo kulikuwa na vijana wengi waliopata nafasi ya kuanza.

Lakini katika mchezo wa marudio uliochezwa jana usiku, Barcelona ikaweka kikosi chake cha kwanza kikiongozwa na Lionel Messi na Luis Suarez huku Phillipe Coutinho ambaye ni mgeni kikosini hapo akiwa jukwaani akishuhudia kila kitu.

Waliofunga mabao katika mchezo huo ni Lionel Messi dakika ya 13 na 15, Jordi Alba dakika ya 28, Luis Suarez dakika ya 31 na Ivan Rakitic dakika ya 87.