Habari za Kimataifa

yayatoure

" Alikuwa ananionea Wivu "

 Yaya Toure amemtuhumu Pep Guardiola kwa kudai kwamba kocha huyo wa Manchester City ana chuki na wachezaji wa Kiafrika.

 Kiungo huyo wa kimataifa wa Ivory Coast ameondoka Manchester City mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kucheza mechi chache sana chini ya Guardiola . Ni kwa mara ya pili Toure kuondoka chini ya Guardiola mara ya kwanza ilikuwa pale Barcelona.

 Toure mwenye umri wa miaka 35 amesema kwamba hakutendewa haki na Guardiola na kuhisi kwamba huenda ni kwasababu ni Muafrika .

 " Nataka kuwa wa kwanza kuvunja hii tabia ya Guardiola ."

 " Nilijaribu kuelewa na hata kuwauliza baadhi ya makocha kuhusu takwimu zangu.Pindi nilipogundua kwamba zilikuwa nzuri kote kwenye mazoezi na mechi , sawa na wale wanaocheza na tena wadogo zangu, nikaelewa kwamba tatizo sio uimara wa kimwili. Sijui kwanini lakini nahisi kwamba alikuwa na wivu , alikuwa ananiona mimi kama mpinzani wake."

 " Ninahisi kwamba Pep, bila kutambua au heshima  alifanya kila kitu kuharibu msimu wangu wa mwisho pale City."

 " Alikuwa mkatili sana kwangu, hivi unadhani angeweza kufanya vile kwa Andres Iniesta?  Ilifikia mahala mpaka nikajiuliza kama sababu ilikuwa rangi yangu. Mimi sio wa kwanza , baadhi ya wachezaji wa Barca wameuliza maswali kama hayo."

 " Ana akili sana kumkamata . Hawezi kukiri kwamba hapendi wachezaji wa Kiafrika. Lakini siku ambayo atachagua kikosi ambacho kina wachezaji watano wa Kiafrika , nakuaidi nitampelekea keki."

 " Zaidi ya hapo Pep anapenda kutawala na kupenda kuwa na wachezaji watiifu wanaombusu mkono . Sipendi mahusiano kama hayo. Naheshimu makocha wangu lakini mimi sio mtumwa wao."

 Toure pia amechukizwa jinsi alivyoagwa ndani ya kikosi cha City na kumtupia lawama Guardiola kwamba yeye ndio aliharibu.

 " Aliiba sherehe yangu ya kuagwa , klabu yenye mashabiki wazuri sana. Nilitamani kuondoka kwa hisia kubwa kama alivyofanya Iniesta au Gianluigi Buffon lakini Pep alizuia kufanyika hivyo."