Habari za Kimataifa

 

Hapo jana dunia ya soka ilipigwa na butwaa na kutoamini kama kweli Arsene Wenger anastaafu kuifundisha Arsenal, klabu aliyoifundisha kwa muda wa miaka 22. Umri ambao kama ni mtoto amezaliwa, akakua na sasa hivi angekua mwaka wa pili chuo kikuu.

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amewastua wengi baada ya kukiri kwamba atastaafu kuifundisha Arsenal mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia kwa muda wa miaka 22.

Wenger (68) aliyejiunga na Arsenal mwaka 1996 kutokea Ufaransa alipokua akifundisha, alitoa habari hiyo kwa kustukiza na kuwaambia wafanyakazi na wachezaji wakati wa mazoezi ya klabu hiyo.

Uongozi wa Arsenal unasemekana uko mbioni kutafuta mbadala wa Wenger baada ya kuachana na timu hiyo. Miongoni mwa mabosi wanaotajwa kuja kuchukua nafasi ya Wenger ni Joachim Low,Thomas Tuchel, pia Brendan Rodgers aliyewahi kuifundisha Liverpoool.

"Baada ya kufikiria na kufanya mazungumzo na uongozi wa timu, nadhani ni muda sahihi wa kuachia ngazi mwishoni mwa msimu"

"Nashukuru kwa kuwa na wasaa wa kuitumikia klabu kwa miaka mingi. Nimeiongoza klabu kwa bidii na uadilifu. Napenda kuwashukuru wafanyakazi, wachezaji, Wakurugenzi na mashabiki ambao wamefanya klabu hii kuwa bora sana. Nawaomba mashabiki kusimama na timu na kuifanya izidi kuwa juu.

"Kwa Mashabiki wote wa Arsenal, lindeni thamani ya klabu. Mapenzi yangu na sapoti ni milele"- Alinukuliwa Arsene Wenger akisema katika taarifa ya kuondoka kwake.