KICHUYA, MKUDE HALI SI SHWARI NDANI YA SIMBA

by Harun, 5 months ago
0

Wakati msafara wa kikosi cha Simba ukiwasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na maisha mengine baada ya kutolewa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, inavyoonekana upepo haujatulia kikosini hapo. Simba ilifungwa bao 1-0 na URA ya Uganda katika mchezo wa michuano hiyo ya Mapinduzi na baadhi ya mastaa walioichezea Simba kisha kubadilishwa wakati wa mapumziko walienda kukaa jukwaani moja kwa moja badala ya kuelekea katika benchi kama ilivyo kawaida. Wachezaji waliobadilishwa na nafasi zao kuchukuliwa na wengine wakati wa mchezo dhidi ya URA ni Shiza Kichuya, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Nicholas Gyan na Mzamiru Yassin. Lakini gumzo kubwa limekuwa juu ya Kichuya na Mkude ambao walionekana kama hawakuwa sawa. Baadaye ilidaiwa kuwa Kichuya alionyesha wazi kutofurahishwa na maamuzi ya benchi la ufundi kumpumzisha wakati Mkude yeye alionekana akipiga stori na baadhi ya wadau jukwaani hapo. Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Simba, Masoud Djuma hakutaka kuweka wazi moja kwa moja juu ya nini kilichotokea zaidi ya kusema aliamua kuwapumzisha wachezaji kadhaa kwa kuwa ratiba ilikuwa ikiwalazimisha wacheze ndani ya kipindi cha muda mfupi. Taarifa za ndani zinadai kuwa Kichuya hakufurahishwa kutolewa katika mchezo huo kama ilivyo kwa Mkude ambaye naye hakufahishwa na kilichotokea.